Muguruza atisha Australian Open baada ya kupanda Mlima Kilimanjaro
Muktasari:
Garbine, 26, alishinda French Open mwaka 2016 na Wimbledon mwaka uliofuatia, lakini baadaye alipotea kwenye mchezo wa tenisi na kujikuta akiwekwa namba 32 huko kwenye viwango vya mchezo huo.
MELBOURNE, AUSTRALIA . BINGWA mara mbili wa Grand Slam, Garbine Muguruza amepanda Mlima Kilimanjaro kutuliza akili yake kwa ajili ya kujiandaa na mashindano ya Australian Open na hilo limekwenda sawa baada ya Alhamisi kutinga raundi ya tatu ya mashindano hayo.
Mrembo huyo Mhispaniola, Garbine, aliyewahi kuwa namba moja duniani kwenye mchezo huo wa tenisi alimshindi Ajla Tomljanovic 6-3, 3-6, 6-3 na sasa atacheza na Muikraine, Elina Svitolina leo Jumamosi.
Garbine, 26, alishinda French Open mwaka 2016 na Wimbledon mwaka uliofuatia, lakini baadaye alipotea kwenye mchezo wa tenisi na kujikuta akiwekwa namba 32 huko kwenye viwango vya mchezo huo.
Alitolewa raundi ya kwanza kwenye mashindano mawili ya Grand Slam yaliyopita, kwenye Wimbledon na US Open, hivyo aliamua kuja kivingine katika kujiandaa na msimu wa 2020.
"Unapopanda mlima unakuwa wewe tu. Hupewi tuzo yoyote, hupewi zawadi yoyote, hupigi picha, hakuna kitu kule," alisema Garbine akizungumzia alipopanda mlima mrefu zaidi Afrika, Mlima Kilimanjaro.
"Ilikuwa changamoto ya kiakili na mwili na nilikwenda kwa ajili ya kutafuta kitu cha kujifurahisha, kitu tofauti nje ya tenisi."
Kwa mtu ambaye hapendi baridi, Garbine alikiri kwamba ilikuwa ngumu na alikaribia kuwa na mawazo tofauti wakati akiwa njiani kupanda kileleni.
"Nilipata shida sana na timu yangu kupanda mlima kuelekea nyuzi joto sifuri na ilikuwa usiku," alisema.
Bado mapema, lakini Gerbine kiwango chake kinaonekana kupanda ndani ya mwaka 2020.
Katika mashindano ya Shenzhen, China mrembo huyo alishinda mechi mbili mfululizo kwa mara ya kwanza tangu aliposhinda kwenyeFrench Open kabla ya kwenda kupoteza hatua ya nusu fainali. Baadaye alilazimika kutoka kwenye mashindano ya Hobart katika hatua ya robo fainali kwa sababu ya kuugua.