Mazembe yawarudisha Tanzania, Ulimwengu, Ambokile
Muktasari:
Tanzania ina wachezaji watatu wanaoitumikia TP Mazembe ambao ni washambuliaji Thomas Ulimwengu, Ramadhan Singano na Eliud Ambokile.
MTANZANIA anayekipiga TP Mazembe, Eliud Ambokile amesema wanasubiri kikao cha mwisho na uongozi wa timu yao ili waweze kurejea nchini baada ya Ligi Kuu ya DR Congo kuvunjwa.
Amesema walipewa taarifa ya wachezaji wa kigeni kurejea makwao baada ya kikao hicho na kwamba endapo kama mipaka itakuwa wazi watakuwa huru kuondoka muda wowote.
"Tuliambiwa ligi imevunjwa hadi hali itakapokuwa shwari kutokana na ugonjwa wa covid 19, hivyo kila mchezaji ataruhusiwa kuondoka kwao baada ya kikao hicho," alisema Ambokile.
Ameongeza kuwa pamoja na kuvunjika kwa ligi nchini humo,programu za mazoezi waliendelea kupewa kama kawaida kwa ajili ya kulinda viwango vyao ili msimu utakaoanza ligi wasianze moja.
Mbali na hilo, amesema tangu mwezi wa tatu walianza kupewa nusu mshahara baada ya mwenyekiti wa timu kuwaomba lengo likiwa ni kwenda kutoa msaada kwa waathirika wa ugonjwa wa covid 19,kitu alichokiri kimetikisa uchumi wake.
"Sio jambo baya lakini maisha yetu yanategemea soka,lazima yapo mambo yatayumba,ukichukulia maisha yakupanga Congo ni ghali tofauti na Tanzania,"amesema.
Amesema akifanikiwa kurejea Tanzania anaona itakuwa afadhari hata akipata nusu mshahara haitakuwa changamoto kubwa kwake kutokana na aina ya maisha yaliopo kuwa tofauti na DR Congo
"Sina maana kwamba najutia ,kutoa ni moyo ila kwa muda huu ambapo kuna mlipuko wa ugonjwa huo,inafaa zaidi tukawa nyumbani ili hali ikikaa sawa tutarejea kwenye mapambano ya soka,"amesema.